Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

WIZARA YA FEDHA YASISITIZA ELIMU YA FEDHA KUKUZA UCHUMI WA NCHI IFIKAPO 2050.

03 Jul, 2026
WIZARA YA FEDHA YASISITIZA ELIMU YA FEDHA KUKUZA UCHUMI WA NCHI IFIKAPO 2050.

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb)(katikati) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Huduma za Hazina, Bw. Nsubili Joshua (wa sita kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Wizara ya Fedha wanaoshiriki kutoa Elimu katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yenye Kaulimbiu ya "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ni Fahari ya Tanzania", yanayofanyika katika viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam.

 

Wizara ya Fedha imebainisha kuwa imeelekeza bajeti yake katika kumwezesha mwananchi kiuchumi, ikilenga kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 kupitia kuimarisha sekta binafsi, kukuza elimu ya juu, na kuongeza uelewa wa masuala ya fedha na kodi kwa umma.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde, wakati akizungumza na vyombo vya habari, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayofanyika katika viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Munde alisema Maonesho ya mwaka huu yameonesha mafanikio makubwa katika matumizi ya mifumo ya kidijitali na maboresho ya huduma, mambo ambayo ni nguzo muhimu katika kusogeza huduma za kifedha karibu zaidi na jamii na kurahisisha shughuli za kiuchumi nchini.

"Wizara ya Fedha imeweka mkazo mkubwa katika kuongeza pato la Taifa na pato la mtu mmoja mmoja kama msingi muhimu wa maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na kufikia uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja na pato la mtu mmoja mmoja kufikia dola 7,000 ifikapo mwaka 2050," alisema Mhe. Munde

Aidha, Mhe. Munde aliwahimiza wananchi kuachana na mifumo ya fedha isiyo rasmi na badala yake watumie taasisi rasmi za kifedha katika shughuli zao za kila siku, hatua inayolenga kuongeza usalama wa fedha zao, uwazi, na kuleta ufanisi wa jumla katika mifumo ya kifedha nchini.

Alisema Wizara pamoja na Taasisi zake inaendelea kutoa elimu ya huduma za fedha pamoja na elimu ya kodi kwa wananchi waliotembelea maonesho hayo waweze kuepuka mikopo isiyo rasmi ijulikanayo kama mikopo umiza ili kuendana kikamilifu na mikakati ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050.

‘’ Kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma za fedha ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi, jambo linalotazamiwa kuwa chachu ya ongezeko la pato la mwananchi mmoja mmoja na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, alisisitiza Mhe. Munde.

Mhe. Munde alipongeza Wizara pamoja na Taasisi zake kwa hatua kubwa zilizofikiwa katika utoaji wa elimu kwa wananchi katika maonesho hayo na kusisitiza kuendelea kufanya maboresho ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa bora zinazokidhi mahitaji ya wananchi kwa ufanisi na kuchangia moja kwa moja katika kukuza pato la Taifa.

Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam, kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, yenye Kaulimbiu ya "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ni Fahari ya Tanzania", ni maonesho ya 50 toka kuanza kwake ambapo yanaambatana na kuadhimisha miaka 50 ya maonesho hayo.

MWISHO.