WATUMISHI WA WIZARA YA FEDHA WAPATIWA ELIMU YA KINGA NA UTAMBUZI WA SARATANI.
Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani Ocean Road imeanza kutekeleza zoezi la utoaji wa elimu kuhusu saratani pamoja na vipimo vya uchunguzi wa awali wa saratani kwa watumishi wa Wizara hiyo ili kuongeza uelewa wa namna ya kujikinga, kutambua dalili za awali na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na ugonjwa huo.
Zoezi hilo litakalohusisha utoaji wa elimu kuhusu saratani mbalimbali, ikiwemo saratani ya matiti, tezi dume na shingo ya kizazi, pamoja na vipimo vya awali linatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 10 hadi 14 Agosti 2026, katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Mtumba, jijini Dodoma.
